Wednesday , 19th Dec , 2018

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amewataka watanzania kuheshimu sheria mbalimbali za nchi ili kuepuka madhara yatakayotokana kwa kutoheshimu sheria hizo.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akikata Utepe na Viongozi mbalimbali wa Serikali na Vyama vya Kisiasa pamoja na Viongozi wa Dini wakati wa hafla ya uwekaji jiwe la Msingi la Ujenzi wa Upanuzi wa barabara ya Morogoro Kuanzia Kimara hadi Kibaha yenye Urefu wa Kilometa 19.2 .Hafla iliyofanyika Kimara Jijini Dar es Salaam.

Ameyasema hayo leo wakati akiweka jiwe la msingi katika mradi wa upanuzi wa njia nane wa barabara ya Morogoro kutoka eneo la Kimara hadi Kibaha mkoani Pwani, yenye urefu wa kilometa 19.2  na kugharimu shilingi bilioni 141.5, uliofanyika Kimara Stop over jijini Dar es salaam,

Rais Magufuli amewataka watanzania kutii na kuheshimu sheria za nchi kwa kutoendeleza maeneo ya hifadhi ya barabara kwani kwa kufanya hivyo ni kukiuka sheria za nchi na kujiletea umaskini.

Watanzania tujifunze kuheshimu sheria, ukisogelea barabara hasa hifadhi ya barabara madhara yake ni umaskini, nataka kuwaambia wananchi waliobomolewa nyumba zao na wakiwemo ndugu zangu ni kwa sababu ya kutoheshimu sheria,” amesema Rais Magufuli.

Pia amefafanua kuwa  Serikali ilitumia fedha nyingi kuweka alama za kuonesha hifadhi za barabara nchi nzima  lakini kwa  bahati mbaya  baadhi ya wananchi hawakutii sheria na kuendeleza maeneo hayo ya hifadhi kwa kujenga nyumba za makazi ama za biashara.

Aidha, Rais Magufuli ameelezea kuwa Sheria ya barabara iliyotungwa mwaka 1932 na kufanyiwa mabadiliko mwaka 1967 imeainisha upana mita 90 kila upande wa barabara kutoka Ubungo hadi Stopover, na kutoka Stopover hadi Kibaha dampo  upana wa mita 121 kila upande, ambapo upana wa barabara hiyo unabadilika  na kupungua mita kadhaa  katika maeneo mbalimbali na  kusisitiza kuwa sheria hiyo  imewekwa makusudi kwa kutambua umuhimu wa barabara hiyo inayounganisha Bandari ya Dar es salaam,  mikoa mbalimbali pamoja na nchi za jirani.