Friday , 6th May , 2016

Rais Magufuli ameagiza kufutwa kwa hati za wamiliki wa mashamba makubwa ambao wameshindwa kuyaendeleza, na kisha mashamba hayo wagawiwe wananchi.

Rais Magufuli ziarani

akizungumza katika miji ya Katesh, Babati, Dareda na Magugu Mkoani Manyara Dkt. Magufuli amepokea malalamiko ya wananchi kuhusu kukosa maeneo ya kuendesha shughuli za kilimo na ufugaji, na amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Manyara Bw. Joel Bendera na wakuu wilaya za mkoa huo kukamilisha mchakato wa kuyapitia mashamba yote yaliyotelekezwa na wamiliki wake, kisha wawasilishe taarifa kwake ili afute hati za umiliki wa mashamba hayo na kuamuru wagawiwe wananchi.

"Kero kubwa katika maeneo haya, pamekuwa na mashamba makubwa ambayo yalichukuliwa na wenye pesa, halafu yale mashamba hawayaendelezi, na wanapoacha kuyaendeleza wanawachukua wananchi masikini na kuanza kuwakodisha, kwa kukusanya fedha, mniachie hili ndugu zangu nitalishughulikia" Amesisitiza Dkt. Magufuli.

Mjini Babati Rais Magufuli amepokea kilio cha wananchi waliodai kudhulumiwa haki zao na kujikuta wakipoteza mali ikiwemo nyumba za kuishi na mazao na amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Manyara kupanga siku za kusikiliza kero za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi.

Rais Magufuli amewasili Mjini Arusha akitokea Dodoma kwa njia ya barabara na kesho anatarajia kutunuku kamisheni kwa maafisa wapya wa Jeshi la wananchi Tanzania (JWTZ) kundi la 58/15 katika chuo cha mafunzo ya jeshi Monduli.