Tuesday , 6th Dec , 2016

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemsimamisha kazi Mhasibu Mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi ya  Ngorongoro (NCAA), Sezzary Simfukwe kwa tuhuma za ubadhilifu wa fedha zinazomkabili na tayari  anahojiwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).

Ofisi za makao makuu ya NCAA

Amefanya maamuzi hayo leo alipotembelea Ofisi za makao makuu ya NCAA, zilizoko wilayani Ngorongoro mkoa Arusha  wakati akizungumza na watumishi wa mamlaka hiyo pamoja na Wajumbe wa  Baraza la Wafugaji ikiwa ni  sehemu ya ziara yake ya kikazi mkoani humo.

"Haiwezekani mtumishi  awe anachunguzwa  na TAKUKURU halafu aendelee kuwa ofisini si atavuruga uchunguzi. Asimamishwe kazi kuanzia leo mpaka hapo uchunguzi utakapokamilika na aikibainika kwamba hana hatia atarudi kazini,” alisema.

Pia Waziri Mkuu alimtaka Mkurugenzi Mkuu wa NCAA, Fred Manongi kueleza zilipo sh. bilioni moja zilizotolewa na Rais wa Awamu ya Nne, Dk. Jakaya Kikwete  kwa ajili ya kujengea ranchi  ya wafugaji wa tarafa ya Ngorongoro.

Akijibu swali hilo Manongi alisema wakati Rais Kikwete anatoa fedha hizo alikuwa bado hajateuliwa kushika washifa huo, ambapo Waziri Mkuu alimuagiza Mkurugenzi huyo  kufanya uchunguzi juu ya fedha hizo na kasha kumpelekea tarifa.