Friday , 17th May , 2019

Mbunge wa Shinyanga Mjini, Stephen Masele ambaye pia ni Makamu wa Rais wa Bunge la Afrika (PAP) ameendelea kushikilia msimamo wake dhidi ya Rais wa Bunge la Afrika, Roger Nkodo Dang licha ya yeye mwenyewe kuitwa na Spika na Bunge Job Ndugai kwa ajili ya kuhojiwa na kamati.

Kupitia ukurasa wake rasmi wa Twitter, Mbunge huyo ameandika jumbe mbalimbali zinazoashiria kumtuhumu Rais wa Bunge la Afrika kuwa anahusika katika unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya wanawake.

"Asanteni kwa kila mtu na msaada alionipa, ninasimamia haki, ukweli, uaminifu na maadili, mimi ni kama mzazi wa mtoto wa kike ninawahasa kila mtu, asivumilie matukio ya unyanyasaji wa kijinsia kwenye shule, maeneo ya kazi na jamii zetu." ameandika Mbunge Masele

Mapema Mei 16, 2019 Bungeni jijini Dodoma, Spika wa Bunge Job Ndugai alitangaza kumsimamisha uwakilishi wa Bunge la Afrika (PAP), kwa madai ya kukosa nidhamu.

"Kwenye Bunge la Afrika (PAP) kumetokea matatizo makubwa kwa Mb. Stephen Masele, na tumelazimika kumrudisha nyumbani kuanzia Jumatatu ila amegoma, hata jana kwenye bunge hilo akihutubia amesema japo ameitwa na Spika anadai ameambiwa na Waziri Mkuu apuuze" alisema Spika Ndugai

"Nimemuandikia barua Rais wa PAP ya kusitisha uwakilishi wake, hadi Kamati ya Maadili itakapokamilisha uchunguzi wa tuhuma dhidi yake, na hapa kuna kamati mbili zinamsubiri ikiwemo Kamati ya Maadili ya Bunge na Kamati ya Maadili ya chama chake." alisema Spika Ndugai.