Sunday , 9th Apr , 2017

Mke wa Rais Mama Janeth Magufuli leo ameadhimisha siku yake ya kuzaliwa kwa kutoa msaada wa vitu mbalimbali kwa wagonjwa katika Taasisi ya Magonjwa ya Saratani ya Ocean jijini Dar es salaam na kutoa wito kwa Watanzania kusaidia watu wenye mahitaji.

Mke wa Rais Mama Janeth Magufuli akimkabidhi zawadi kwa mmoja wa wagonjwa katika kusherehekea siku yake ya kuzaliwa na   wagonjwa waliolazwa katika Taasisi ya saratani ya Ocean Road jijini Dar es salaam

Akiwa hospitalini hapo, Mama Magufuli, amesema ameamua kuwatembelea na kuwafariji wagonjwa hospitalini hapo kwa kutoa msaada huo kwa kuwa yeye alizaliwa katika hospitali hiyo tarehe na mwezi kama wa leo ambapo pia alipata fursa ya kuwaombea afya njema wagonjwa wote na kuwatia moyo ndugu wanaouguza kuendelea na jukumu hilo zito.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, Dk. Julius Mwaisalage amemshukuru s Mama Janeth Magufuli kwa moyo wake wa kujitolea kwa kusaidia wagonjwa hospitalini hapo kwa kuwa kitendo hicho kinawatia moyo wao kama wauguzi lakini pia kinarudisha imani kwa wagonjwa na kujiona kuwa hawapo peke yao.

Mke wa Rais Mama Janeth Magufuli akimkabidhi Mkurugenzi wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road Dkt. Julius Mwaisalage misaada ambayo ametoa kusherehekea siku yake ya kuzaliwa kwa  wagonjwa waliolazwa katika Taasisi hiyo jijini Dar es salaam.

Mama Janeth Magufuli kwa kushirikiana na wanawake wa Wilaya ya Ilala na Temeke wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Ilala Sophia Mjema wametoa msaada wa vitu mbalimbali kama vile mchele, maharage, sabuni za kufulia, sabuni za kuogea, maziwa ya unga,juisi, taulo za kike, vitenge, kanga, misuli,mafuta ya kujipaka na dawa za meno.

Mke wa Rais Mama Janeth Magufuli akisalimia ndugu waliofika kuona wagonjwa  alipotembelea  Taasisi ya Saratani ya Ocean Road   jijini Dar es salaam na kusherehekea siku yake ya kuzaliwa kwa kutoa misaada kwa wagonjwa waliolazwa katika hospitali hiyo ambako ndiko alikozaliwa yeye.