Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora - Bahame Tom Nyanduga
Akizungumza wakakati wa ufunguzi wa kongamano lililoandaliwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, (LHRC), Kamishina wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora nchini ,Tom Bahame Nyanduga amesema, serikali inapaswa kuangalia upya sheria hiyo kwa sababu ni kandamizi na ni ya kikoloni.
Nyanduga amesema, mpaka sasa nchi zaidi ya ishirini barani Afrika zimeshafuta sheria hiyo na nchi kama za Umoja wa Ulaya na Canada sheria hiyo haitumiki ,hivyo serikali inapaswa kuangalia upya namna ya kufuta adhabu ya kifo kwakuwa haitekelezeki.
Ameongeza kwamba, adhabu hiyo ipo kinyume na haki za binadamu na inapingana na katiba ya nchi inayosema kila mmoja ana haki ya kuishi na ikitekelezwa haina adhabu mbadala na kuwafanya watu kuishi kwa wasiwasi wakiwa magerezani.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Dk. Hellen Kijo Bisimba, amesema, adhabu hiyo inatekelezwa kwa makosa ya Mauaji, Uhaini na wanajeshi ambao wameasi nchi na kwenda kinyume na taratibu na kanuni za majeshi na kwamba, kwa mujibu ya maoni ya wadau na wananchi ni asilimia 50% pekee ndiyo waliomba kuendelea kuwepo kwa adhabu hiyo huku wengine wakikataa.