Saturday , 27th Jun , 2015

Jeshi la polisi Mkoani Morogoro limesema linawashikilia vijana 6 waliokamatwa kufuatia msako uliofanywa na Jeshi hilo katika msitu wa Kilindu katika mipaka ya mikoa ya Morogoro,Tanga na Pwani.

Akizungumza na East Africa Radio kwa njia ya Simu, Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro Mussa Marambo amesema baada ya kuwepo taarifa za vijana zaidi ya 50 kufanya uhalifu katika maeneo hayo, jeshi hilo liliamua kuzifanyia kazi kwa kufanya msako katika mitu huo, na kufanikiwa kukamata vijana sita.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mussa Marambo amesema hakuna mtu aliyeuawa katika mapambano hayo tofauti na taarifa za awali zilizodai kuuawa kwa watu watatu miongoni mwao wawili wakidhaniwa kuwa ni magaidi wa Al Shabaab.

Awali Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Morogoro katika mkutano na waandishi wa habari alisema tukio hilo limetokea eneo la mpakani mwa mkoa wa Morogoro wilaya ya Mvomero na mkoa wa Tanga ambapo watu hao walikuwa wamejificha msituni.

Amesema jeshi hilo linawashikilia watu sita kwa kuhusika na tukio hilo, na kwamba uchunguzi zaidi unafanyika ikiwa ni pamoja na msako mkali katika eneo hilo.

Taarifa kutoka katika hospitali ya mission ya Turian mkoani Morogoro zinasema kuwa maiti tatu zimehifadhiwa hapo ambapo kati ya hizo, maiti mbili zinaonekana kuwa ni za watu wasio raia wa Tanzania huku moja ikiwa ni ya mtu ambaye alijeruhiwa vibaya na badaye kufariki akiwa hospitalini hapo.

Licha ya jeshi la Polisi kukanusha, uchunguzi uliofanywa na mwandishi wetu umethibitisha kuwepo kuwepo kwa vifo hivyo ambapo matron wa hospitali ya mision ya Turian amethibitisha kupokea maiti 3, 2 kati ya hizo zikisadikiwa kuwa ni za watu wasio raia wa Tanzania.

Akikanusha taarifa hizi kwa njia ya simu ACP Marambo amesema hakuna aliyejeruhiwa zaidi ya askari mmoja aliyekatwa na kisu cha mmoja wa vijana hao mkononi, na hapa anaeleza zaidi, msikilize.......

Sauti ya Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Morogoro, ACP Musa Marambo