Saturday , 24th Nov , 2018

Jeshi la Polisi Mkoani Iringa limekataa ombi la kufanya mkutano wa hadhara ulioitishwa na Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini Mchungaji Peter Msigwa, kwa kile ilichokieleza kutokuwa na ulinzi wa kutosha.

Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini Mchungaji Peter Msigwa.

Kwa mujibu wa barua iliyoandikwa na Jeshi hilo kwenda kwa Mbunge Msigwa, imeeleza kuwa polisi wamepokea taarifa za kiintelijensia ikieleza kuwa wamegundua uwepo wa vikundi vya watu ambao wamepanga kufanya vurugu kwenye mkutano huo.

Aidha sababu nyingine iliyoelezwa na Jeshi la Polisi,  imedai kuwa imezuia mkutano huo kwa kutokuwa na askari wa kutosha ambao wengi wameelekezwa kwenda kusimamia, mitihani ya kidato cha nne na kidato cha pili.

Kwa mujibu wa barua ambayo aliandika Mchungaji Msigwa Novemba 19, Mbunge huyo alihitaji kufanya mkutano huo katika uwanja wa Mwembetogwa ambapo alihitaji uanze saa 8 mchana hadi saa 12 jioni.

Oktoba 9 mwaka huu akizungumza na www.eatv.tv, Msigwa alisema kuwa "Nilishikiliwa na Polisi kwa muda nikitakiwa kutoa maelezo kwa kile walichodai kuwa nimetoa lugha ya uchochezi kwenye mkutano wa hadhara lakini sikufanya hivyo nimegoma na wakasema wataniita wakinihitaji tena".