Monday , 10th Oct , 2016

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, leo amepokea hati za utambulisho za mabalozi wanne wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika picha ya pamoja na Balozi mteule wa Jamhuri ya Sudan hapa nchini Mahjoub Ahmed Abdallah Sharfi mara baada ya kupokea Hati yake ya utambilisho Ikulu jijini Dar es Salaam.

Mabalozi waliowasilisha hati zao za utambulisho Ikulu Jijini Dar es Salaam ni Balozi wa Jamhuri ya Sudan Mhe. Mahjoub Ahmed Abd Allah Sharfi, Balozi wa Jamhuri ya Slovakia Mhe. Frantisek Dlhopolcek, Balozi wa Ukraine Mhe. Yevheni Tsymbaliuk na Balozi wa Jamhuri ya Ghana Mhe. Kwame Asamoah Tenkorang.

Rais Magufuli amezungumza na Mabalozi hao kwa nyakati tofauti baada ya kupokea hati zao za utambulisho, ambapo wamesisitiza umuhimu wa kuendeleza na kuimarisha uhusiano na ushirikiano kati ya Tanzania na nchi hizo kwa kujikita zaidi katika biashara na uwekezaji.

"Mhe. Balozi najua nchi yenu ya Sudan ina utajiri wa mafuta na imefanikiwa kujenga uchumi wake kupitia mafuta, sisi pia hapa nchini tumebaini uwepo wa mafuta na gesi asilia katika maadhi ya maeneo, ningependa uhusiano na ushirikiano wetu sasa ujielekeza katika kubadilishana uzoefu na ujuzi wa namna tunavyoweza kunufaika na mafuta na gesi" amesema Rais Magufuli alipokuwa akizungumza na Balozi wa Sudani hapa nchini Mhe. Mahjoub Ahmed Abd Allah Sharfi.

Dkt. Magufuli pia ametoa wito kwa wafanyabiashara na wawekezaji kutoka nchi za Sudan, Slovakia, Ukraine na Ghana kuja kuwekeza hapa nchini katika sekta mbalimbali zikiwemo Mafuta na gesi, Kilimo, Uvuvi, Mbuga za wanyama, Madini na ufugaji.

"Hivi sasa Tanzania ipo katika mpango wa ujenzi wa viwanda na pia tunatekeleza mpango wa pili wa maendeleo, hivyo nakuomba Mhe. Balozi uwahamasishe wafanyabiashara na wawekezaji wa Ukraine waje wawekeze katika viwanda kwani soko la uhakika la bidhaa lipo" amesisitiza Dkt. Magufuli alipokuwa akizungumza na Balozi wa Ukraine hapa nchini Mhe. Yevheni Tsymbaliuk.

Aidha, Rais Magufuli amewasihi Mabalozi wa Slovakia, Ukraine na Ghana ambao makazi yao ya Ubalozi yapo Mjini Nairobi nchini Kenya kuanzisha Ubalozi wao hapa nchini ili kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano katika masuala ya biashara na uwekezaji.