Tuesday , 6th Sep , 2016

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amehidi kumalizia kiasi cha shilingi bilioni tano alichoahidi katika ujenzi wa mabweni ya wanafunzi wa chuo kikuu cha Dar es Salaam na kuahidi ajira kwa watendaji wa ujenzi huo.

Rais Magufuli zakizungumza na mafundi na wakandarasi wanatekeleza ujenzi wa mabweni ya wanafunzi, UDSM

Rais Magufuli amekagua maendeleo ya ujenzi wa mabweni ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ikiwa ni utekelezaji wa ahadi aliyoitoa kwa chuo hicho alipokwenda kuweka jiwe la msingi katika ujenzi wa maktaba ya kisasa ya chuo hicho tarehe 02 Juni, 2016.

Jumla ya majengo 20 yenye ghorofa nne kila moja yanajengwa katika eneo hilo la mashariki mwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na yatakapokamilika tarehe 31 Desemba, 2016 yatakuwa na uwezo wa kuchukua wanachuo 3,840 kati ya wanachuo 7,000 wanaolazimika kupanga vyumba vya kuishi mitaani kutokana na kukosa nafasi katika mabweni ya chuo yaliyopo.
Akizungumza na wafanyakazi wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) na Vijana walioajiriwa katika kazi za ujenzi wa majengo hayo Rais Magufuli amepongeza moyo wa uzalendo waliouonesha kwa kufanya kazi usiku na mchana na amemuagiza Mtendaji Mkuu wa TBA Elius Mwakalinga kuendelea kuwatumia vijana hao katika miradi mingine ambayo Serikali itaitekeleza kwa kutumia TBA.

TBA ikitumia wataalamu na Vijana wa Kitanzania itatumia Shilingi Bilioni 10 kukamilisha ujenzi huo ikilinganishwa na endapo ingetumia Wakandarasi ambao walitaka kulipwa kati ya Shilingi Bilioni 50 na Bilioni 100.

Rais Magufuli ameutaka uongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuacha kuingia mikataba mingine na wafanyabiashara wanaotumia maeneo ya chuo hicho kujenga majengo ya kibiashara na badala yake amesema Serikali itaendelea kutafuta namna ya kulimaliza tatizo la mabweni kwa wanafunzi wa chuo hicho na vyuo vingine hapa nchini.

Majengo ya mabweni yanayotarajiwa kukamilika hivi karibuni