Thursday , 27th Oct , 2016

Tanzania imetajwa kufanya vizuri kiuchumi kwa mujibu wa ripoti ya hali ya uchumi barani Afrika.

Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe. Charles Mwijage

Katika ripoti hiyo imebainika kuwa kiwango cha mfumuko wa bei nchini kipo chini pamoja na kuimarika kwa thamani ya shilingi huku uchumi ukikua kwa kasi ya zaidi ya asilimia saba kwa mwaka.

Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe. Charles Mwijage amesema hayo leo jijini Dar es Salaam, wakati wa utoaji wa ripoti hiyo iliyoandaliwa na Benki ya Maendeleo Barani Afrika AfDB ambapo hata hivyo amesema bado jitihada zinahitajika katika kuleta mageuzi yatakayosaidia kuongeza tija kwenye sekta ya kilimo.

Baadhi ya maeneo ambayo Tanzania haijafanya vizuri ni katika udhibiti wa ukuaji holela wa idadi ya watu wanaohama kutoka vijijini na kukimbilia mijini huku jiji la Dar es Salaam likiongoza kwa kupokea watu laki mbili na nusu kwa mwaka.

Kufuatia hali hiyo Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bi. Angelina Mabula ameeleza hatua zinazochukuliwa kukabiliana na hali hiyo kuwa ni utekelezaji wa mpango wa matumizi bora ya ardhi kupitia mradi ujulikanao kama Land Tenure.