Thursday , 13th Oct , 2016

Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imetangaza kupunguza kodi mbalimbali za ardhi ili kuwawezesha wananchi wengi hasa wanaoishi katika maeneo yasiyo rasmi ili kufanikisha mpango wa urasimishaji wa ardhi kwa wakazi wa maeneo hayo.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Wiliam Lukuvi.

Hatua hiyo imetangazwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Wiliam Lukuvi Mkoani Mwanza wakati akiongea na wataalam na viongozi wanaosimamia sekta ya ardhi mkoani humo.

Mhe. Lukuvi amesema kuwa takwimu zinaonyesha kuwa Mwanza ni mji unaokua kwa kasi ya asilimia 13 kwa mwaka ukuaji ambao umekuwa na mahitaji makubwa ya viwanja vya makazi na biashara na kusababisha zaidi asilimia 70 ya wakazi wa Mwanza kuishi katika makazi holela.

Waziri Lukuvi amesema kutokana na hatua hiyo na kuzingatia hali ya uchumi wa mtanzania katika kumiliki ardhi walikuwa wanatozwa kodi kubwa ambayo ilikuwa inawafanya wanashindwa kupata hati ya kumiliki ardhi hivyo serikali imeliangalia suala hilo kwa mapana zaidi.

Aidha Waziri huyo amebainisha suluhishi la kupunguza uhaba wa wataalamu wa upimaji wawatume wapangazi na wapimaji binafsi waliodhinishwa na Wizara yake ili kufanikisha zoezi hilo kwa urahisi na haraka zaidi.