Monday , 5th Sep , 2016

Serikali imesema imejizatiti katika kuwaandaa na kuwatafuta wataalam wa kilimo hasa wenye uwezo kuhusu maswala ya ukaushaji wa mazao ya nafaka ili kukabiliana na changamoto zinazosababishwa na tatizo la unyevunyevu kwenye mazao hayo.

Charles Mwijage

Kauli hiyo imetolewa na waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Charles Mwijage kwenye mahojiano maalum na East Africa TV, ilipotaka kujua ni jitihada gani ambazo zinachukuliwa na serikali katika kutatua malalamiko ya wakulima wa nafaka kuhusu kuharibika kwa mazao yao kwa sababu ya tatizo la unyevunyevu ambalo limekuwa likiwaletea hasara kubwa wakulima wa nafaka nchini na kushindwa kufikia masoko ya kimataifa kiushindani.

Waziri Mwijage amesema wizara yake imejiwekea malengo katika kuwasaidia wakulima wa nafaka kwa kuwatafutia vifaa vya kisasa ambavyo vitapatikana kwa gharama nafuu ili kuhakikisha mazao hayo yanayolimwa nchini yanakwenda kuuzwa kwenye masoko ya kimataifa ili kuiwezesha fedha ya Tanzania kupanda zaidi kwenye masoko ya kimataifa na kuongeza pato la mtu mmojammoja na taifa kwa ujumla.

Amesema kutokana na ushindani uliopo kimataifa serikali imedhamiria kuwasaidia wakulima kwa kuwapa miongozo kitaalam na kutafuta fedha za kununua mashine maalum zakukaushia mazao ya nafaka pindi yanapovunwa mashambani ili kuyawezesha kiushindani na mazao kutoka nchi nyingine.