
Hayo yamesemwa leo Bungeni mjini Dodoma na Naibu Waziri, Wizara ya Nishati na Madini, Mhe. Medard Kalemani wakati akijibu swali na Mbunge wa Jimbo la Biharamlo Magharibi kuhusu mikakati ya Serikali ya kuwaunga mkono wachimbaji wadogo wadogo wa Busiri.
Mhe. Kalemani ameeleza kuwa hadi mwisho wa mwezi Machi, 2016 Wizara yake imegawa kwa wananchi wa Busiri leseni 81 za uchimbaji mdogo wa madini katika eneo hilo, sawa na takribani hekta 810 kati ya hekta 11,031 za eneo lililoachwa kwa ajili ya wachimbaji wadogo.
Ameongeza kuwa mkakati mwingine wa Serikali ni kuendelea kulitumia Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kutoa huduma ya ugani kwa wachimbaji madini wadogo wa kijiji cha Busiri na wengine wote nchini ikiwemo kutoa ruzuku kupitia mfuko wa wachimbaji wadogo.
Aidha, Serikali imekuwa ikiwatembelea wachimbaji madini wa eneo hilo mara kwa mara kutumia maafisa na wataalamu wa ofisi ya kanda ya ziwa Viktoria Magharibi na ofisi ya Afisa Madini mkazi-Bukoba.