Monday , 5th Sep , 2016

Tanzania imeanza kutumia sheria mpya ya kuwalinda watoa taarifa za uhalifu na makosa pamoja na mashahidi wa makosa mbalimbali waliyoshuhudia yakitendeka kwa kuwapatia ulinzi wa kisheria ili kuongeza mapambano dhidi ya uhalifu nchini.

Dkt Harrison Mwakyembe

Wizara ya Katiba na Sheria imeeleza hayo leo Jijini Dar es Salaam, kupitia Mkurugenzi wa Utekelezaji wa Katiba Bw. Kamana Stanley wakati akielezea juu ya sheria hiyo ambayo itawawezesha wananchi na mashuhuda kuelezea matukio ya uhalifu na matendo yanayofanywa kinyume cha sheria.

Hatua hiyo itaisaidia serikali katika mapambano dhidi ya uhalifu na kujenga jamii na taifa linalopinga uhalifu sambamba na kukuza ari ya wananchi kusimamia wenyewe katika kuokoa mali ya umma, kulinda mazingira na maisha ya binadamu kutokana na uhalifu uliopangwa kufanyika.

Muswada huo ulipitishwa na kuwa sheria ya kuwalinda watoa taarifa za uhalifu na mashahidi ambayo kwa kiingereza inajulikana kama (The Whistleblower and Witness Protectin Act. 2016) na kutangazwa katika gazeti la serikali kupitia tangazo Na. 110.

Aidha Mhe. Dkt Harrison Mwakyembe ambaye ni Waziri mwenye dhamana ya usimamizi wa sheria husika aliidhinisha Julai Mosi, 2016 kuwa ndiyo siku ya kuanza kutumika kwa sheria hiyo.