Thursday , 27th Dec , 2018

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameamua kuitisha kikao cha Mawaziri wote na makatibu wakuu wote kesho (Ijumaa) saa 5 asubuhi ili waeleze kazi hiyo ya ujenzi wa majengo ya serikali itakamilishwa lini.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa

Ametoa kauli hiyo leo (Alhamisi, Desemba 27, 2018) mara baada ya kukagua ujenzi wa ofisi za wizara zote pamoja na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika eneo la Mtumba lililoko km. 17 kutoka jijini Dodoma.

Nimekagua maeneo yote na kukuta baadhi ya wakandarasi wanatakiwa kujenga majengo ya wizara nne hadi tano, sijaridhika na baadhi ya kazi, nimeitisha kikao cha Mawaziri wote kesho ili tuangalie ni mkandarasi yupi anaweza kumudu hii kazi.”

Nimebaini kuna tatizo kubwa la upatikanaji wa vifaa vya ujenzi kama kokoto, nondo, matofali na kikao cha kesho kitahusisha Mawaziri, Makatibu Wakuu, viongozi wa Mkoa na Jiji la Dodoma, wakandarasi wote ili tukubaliane kazi hii inaisha lini,” amesema.

Akisisitiza uharaka wa kazi hiyo, Waziri Mkuu amesema kazi hiyo ina malengo maalum na inatakiwa ikamilike haraka sana.