
Mkuu wa Wilaya ya Iringa Richard Kasesela, akiwa katika kipindi cha HOT MIX
Kasesera ameyasema hayo alipokuwa akizungumza katika kipindi cha HOTMIX kinachorushwa na EATV, ambapo ameweka wazi kwamba anafanya kazi yake ya kuwatumikia wananchi na ofisini hushinda mara chache sana ili kuonana na wananchi na kutatua kero zao katika maeneo yao.
“Mimi sina mbwembwe, mfano zile picha zinazoonesha nikiwa kwenye maji nikiokoa watoto, kule mvua ilinyesha kitongoji kizima kikawa kinatakiwa kuokolewa ikabidi niende na viongozi wenzangu kufanya uokozi na Mungu alisaidia tukafanya vyema” Amesema Kasesela
Aidha Kasesela ameongeza kuwa baada ya kuteuliwa kwa mara ya kwanza na Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Kikwete aliingia kazini moja kwa moja hivyo hakuwahi kupata semina ya ukuu wa wilaya, na alipoteuliwa na Rais Dkt. John Magufuli akawa tayari amepata uzoefu wa kuendelea kutumikia umma.
Pamoja na hayo DC Kasesela amewataka viongozi wa umma kutumia mitandao ya kijamii kwani imekuwa ikitoa taarifa mbalimbali kuhusu kero za wananchi.
‘Mimi natumia mitandao ya kijamii mingi, hasa facebook imekuwa ikinisaidia sana ambapo watu hunitumia ujumbe mfupi ‘meseji’ na nikifuatilia mambo hayo mara nyingi huwa ni kweli na kuyatatua kwa haraka.
Wakati huo huo DC Kasesela amesema hana ugomvi na viongozi wa UKAWA katika wilaya yake na anafanya nao kazi kwa ushirikiano kwani anatekeleza kwa vitendo falsafa ya ‘hapa kazi tu’.
