Thursday , 20th Oct , 2016

Serikali kupitia Wakala ya Serikali Mtandao (eGA) imeendelea kutekeleza uunganishwaji wa mtandao wa Mawasiliano wa Serikali ambapo mpaka sasa Taasisi 72 zimeunganishwa na mtandao huo.

Meneja wa Habari, Elimu na Mawasiliano wa eGA, Suzan Mshakangoto

 

Hayo yamebainishwa na  Meneja wa Habari, Elimu na Mawasiliano wa eGA, Suzan Mshakangoto alipokuwa akieleza kuhusu utekelezaji wa miundombinu ya Tehama inayohusisha Serikali, leo Jijini Dar es Salaam.

Bi. Suzan amesema, Taasisi za Serikali zilizounganishwa na mtandao huo zitakuwa zinawasiliana kwa gharama ndogo kwa kutumia simu zitakazokuwa zikitumika kama ‘extension’ ambazo zitakuwa zinatumia internet kupitia Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano.

Ameongeza kuwa, Taasisi za Serikali zitapunguza gharama za huduma za internet kutoka kwa watoa huduma binafsi ambao gharama zao ziko juu ukilinganisha na huduma inayotolewa na wakala wa Serikali.

Aidha Taasisi na Idara zote za Serikali zitakuwa ndani ya mtandao na mtoa huduma mmoja wa huduma za mtandao ambapo itasaidia kwenye utunzaji wa nyaraka za Serikali na kurahisisha mawasiliano ndani ya taasisi hizo.