Monday , 2nd May , 2016

Chama wa Mawakala wa Forodha nchini Tanzania TAFFA kimesema tishio linalotokana na kupungua kwa m

Chama wa Mawakala wa Forodha nchini Tanzania TAFFA kimesema tishio linalotokana na kupungua kwa mizigo inayoingia na kutoka nchini kupitia bandari mbali mbali nchini hivi sasa lipo dhahiri na kwamba kuna haja ya serikali kutodharau tishio hilo na badala yake ichukue hatua za haraka kutokana na madhara ya tishio hilo kwa uchumi wa nchi.

Rais wa TAFFA Bw. Steven Ngatunga amesema hayo leo katika mahojiano na East Africa Radio na kutaja sababu za kupungua kwa mizigo hiyo kuwa ni kutokana na matumizi ya sheria alizodai kuwa sio rafiki kwa mazingira ya biashara na zinazokimbiza wateja hasa wale wanaotoka nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Zambia, Rwanda, Burundi na Malawi.

Bw. Ngatunga amefafanua kuwa ushahidi unaonekana hata katika maeneo ya mipakani na kwamba kupungua kwa mizigo kumeathiri takribani ajira elfu kumi zinazotokana na mnyororo mzima wa usafirishaji mizigo kati ya bandari ya Dar es Salaam na maeneo ya mipakani.