Wednesday , 2nd Nov , 2016

Menejimenti ya Shirika la Posta nchini inakusudia kuchukua hatua za kinidhamu ikiwa ni pamoja na kuwafukuza kazi na kuwafikisha mahakamani, baadhi ya watumishi wake.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Posta Dkt. Haroun Kondo (katikatika) akifafanua jambo kuhusu utendaji mbovu unaolikabili shirika hilo

Watumishi hao ni wale ambao wamehusika katika ubadhirifu wa fedha na rasilimali za shirika hilo, pamoja na utendaji mbovu kiasi cha kusababisha shirika hilo lijiendeshe kwa hasara.

Hatua hizo ni sehemu ya mageuzi makubwa yaliyotangazwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika hilo, Dkt Haroun Kondo, katika mkutano wake na wanahabari leo Jijini Dar es Salaam, muda mfupi kabla ya kuanza kwa kikao cha bodi na watendaji wakuu wa shirika hilo, kikao kinacholenga kuweka mwelekeo mpya na mageuzi yatakayoliwezesha shirika hilo kujiendesha kibiashara.

Dkt. Kondo ametaja baadhi ya maeneo ambayo ni kichaka cha ubadhirifu kuwa ni kwenye mikataba ya kilaghai ambayo shirika hilo imeingia na wadau wake wa kibiashara, na hapa anaeleza namna watumishi wasio na uzalendo walivodiriki kufanya kile alichokiita kuwa ni hujuma za makusudi dhidi ya shirika hilo.