Thursday , 21st Jan , 2016

Imeelezwa kuwa mazungumzo kuhusu nauli za mabasi yaendayo haraka Dar es salaa kati ya UDA na serikali yafikia hatua nzuri.

Uongozi wa Shirika la Usafiri jijini Dar es Salaam – UDA, umesema mazungumzo yanaendelea vizuri baina ya kampuni hiyo na serikali, kuhusu viwango vya nauli vinavyopaswa kutozwa kwa abiria watakaosafiri chini ya mradi wa Mabasi yaendayo haraka jijini Dar es Salaam wa UDA-RT unaotarajia kuanza hivi karibuni....

Afisa Mtendaji Mkuu wa Shirika hilo Bw. Robert Kisena amesema hayo jijini Dar es Salaam leo, katika mkutano wake na waanahabari, ambapo ametetea viwango vya nauli walivyopendekeza hapo awali.

Amesema kuwa viwango hivyo ni sahihi na kwamba vinatokana na waendeshaji wa mradi kuhusika moja kwa moja na gharama za mradi, tofauti na nchi nyingine ambapo miradi kama hiyo inapata ruzuku kutoka serikalini.

Aidha, Kisema ametumia fursa hiyo kusahihisha taarifa zinazosambazwa kupitia mitandao ya kijamii pamoja na baadhi ya vyombo vya habari, ambazo zinaihusisha familia ya Rais mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete na umiliki wa kampuni hiyo ya usafirishaji, kitendo alichodai kuwa kinalenga kuichafua kampuni hiyo pamoja na hadhi ya Rais huyo mstaafu.