Monday , 29th Jun , 2015

Waajiri wa sekta mbalimbali nchini Tanzania wameaswa kuzingatia utekelezaji wa sera ya afya katika maeneo ya kazi ili kukabiliana na tishio la magonjwa yakiwemo UKIMWI na magonjwa mengine ya kuambukiza.

Akizungumza jijini Dar es salaam Mkurugenzi wa Taasisi inayojishuhulisha na utekelezaji wa sera za afya THA Bw Justine Mahimbo amesema kuwa wafanyakazi wanakabiliwa na tishio la magonjwa yasiyoambukiza kama vile saratani, ugonjwa wa moyo na kisukari pamoja na magonjwa ya mtindo wa maisha.

Mahimbo amesema mpaka sasa ni taasisi chache zinazozingatia sera ya afya ikiwemo kuwekeza katika vitengo vinavyosaidia katika utoaji wa huduma za ushauri na kutokana na hilo tatizo la magonjwa yakuambukizwa na yasiyoambukizwa yatazidi kuongezeka.

Ameongeza kuwa miongozo elekezi ya kitaifa na sera zimetungwa zikiwa na lengo la kuwekeza zaidi kinga na matunzo ya VVU, UKIMWI na magonjwa yasiyoambukiza.

Kwa upande wake mmoja wa wamiliki wa taasisi binafsi jijini Dar e s Salaam Robert Lukelo amesema waajiri wengi wanatambua athari ya VVU, UKIMWI, magonjwa yasiyoambukizwa na magonjwa mengine lakini kutokana na kutoona umuhimu wa utekelezaji wa sera hiyo imekuwa ikiachwa.

Lukelo amesema sera ya afya mahali pa kazi ni muhimu na kuwa itasaidia ongezeko la matumizi ya fedha kwaajili ya matibabu, kuongeza hari ya ufanyaji kazi na gharama za mazishi. Na kutaka waajiri kuzingatia suala hilo kuwa mahali pa kazi ni mahali panapofaa kwa ajili ya elimu ya afya na upimaji.

Sera ya Taifa ya Kudhibiti UKIMWI ya mwaka 2012, Mkakati wa Taifa wa Kudhibiti UKIMWI (2013 – 2017) na Mkakati wa Taifa wa Magonjwa yasiyoambukizwa (2009 – 2015) zinahimiza sekta zote zishirikiane kuyakabili magonjwa haya kwa pamoja.