
Tani hizo 3700 za tumbaku inadaiwa kuwa zilikuwa zimekosa wanunuzi kwa sababu na hivyo kuhitaji utatuzi wa haraka wa Serikali ili kuinusuru tumbaku hiyo ambapo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa serikali tayari imefanikiwa kuongea nao na wanunuzi na tani zote zitanunuliwa.
Waziri Mkuu alitoa ahadi hiyo jana jioni Agosti 9, 2017 wakati akizungumza na wadau wa zao la tumbaku zaidi ya 600 wakiwemo wabunge, viongozi wa dini, chama na Serikali kwenye mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Isike-Mwanakiyungi, mjini Tabora.
Waziri Mkuu amewashukuru wanunuzi kumaliza tatizo hilo na wakulima ambapo amesema kuwa kwa sasa wakulima hao watapata hari mpya hari mpya kwa wakulima na kuwafanya wajipange vizuri kwa msimu ujao.
"Makampuni ya ununuzi yatapita kwenye maeneo yenu, WETCU watafuatilia na tumekubaliana nao kuwa tutafanya kazi pamoja," alisema Waziri Mkuu.
Kufuatia sintofahamu hiyo, wiki iliyopita, wakazi wa mkoa huo waliomuomba Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli aingile kati ili kuwanusuru na adha ya zao hilo kukosa soko. Naye akawaahidi wananchi hao kwamba suala hilo atalikamilisha Waziri Mkuu.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Wabunge wa Mkoa wa Tabora ambaye pia ni mbunge wa Urambo, Mheshimiwa Margareth Sitta aliiomba Serikali ikubali kuliangalia suala hilo la tani za ziada 3,700 kwani wakulima wamejaza tumbaku majumbani mwao na kwenye maghala.
"Wakulima wetu wanahitaji kuuza hii tumbaku ili wapate fedha za kuanzia msimu ujao wa kilimo. Lakini pia tunaomba liangaliwe suala la upangaji madaraja ya tumbaku, wasaidiwe kukabili bei isiyotabirika na kutatua ukosefu wa soko la uhakika," alisema Mama Sitta.