Mtandao wa wanafunzi nchini Tanzania Unamuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dakta John Pombe Magufuli kuwachukulia hatua wale wote waliodahili wanafunzi wasio na sifa katika programa maalum iliyoanzishwa katika chuo kikuu cha Dododma na sio kuwaadhibu wanafunzi wote ambapo wengine hawakuwa na hatia.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa mtandao huo Bw Alphonce Lusako alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari hii leo jijini Dar es salaam na kuongeza kuwa Rais amesema baadhi ya wanafunzi walidahiliwa wakiwa hawana sifa za kujiunga na program hiyo mtandao unaona kosa hilo ni la wadahili na sio la wanafunzi hivyo wanafunzi wenye sifa wangeachwa waendelee na masomo yao kama kawaida.
Bw Lusako amebainisha kuwa kutokana na sakata hilo wanafunzi wengi wameathirika kisaikolojia na kukata tamaa wasijue nini cha kufanya huku wengine kujilaumu kujiunga na programu hiyo amabapo wangeendelea na kidato cha Tano wangekuwa wanamaliza kidato cha sita hivi sasa.
Aidha kwa upande wake Mwanafunzi ambae ni muhanga wa sakata hilo, Ibrahim Abdalah amesema kuwa wanasikitika kuona hata walioanzisha programa hiyo wanashindwa kujitokeza kuwatetea kwani hawakwenda kujiunga na program huiyo kwa ridhaa zao bali ni serikali iliamua kuanzisha program hiyo ili kukabiliana na upungufu wa walimu wa sayansi nchini.

