Friday , 6th May , 2016

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amesema wafanyabiashara wote wanaoficha sukari ni wahujumu uchumi na ikipatikana sukari yao wananchi watagawiwa bure.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewataka wafanyabiashara wote walioficha sukari katika maghala yao, kuanza kuisambaza mara moja, vinginevyo serikali itachukua hatua kali ikiwa ni pamoja na kuinyang'anya sukari hiyo na kuisambaza kwa wananchi bure.

Rais Magufuli ametoa maagizo hayo leo tarehe 06 Mei, 2016 katika mikoa ya Singida na Manyara wakati akizungumza na wananchi kwa nyakati tofauti waliosimamisha msafara wake uliokuwa ukitoka Dodoma kwenda Arusha.

Dkt. Magufuli ameviagiza vyombo vya dola kuwafuatilia wafanyabiashara wanaofanya njama za kuficha sukari na kusababisha upungufu wa bidhaa hiyo, na ameapa kuwa serikali yake itawachukulia hatua kali watakaobainika kufanya hivyo.

Pamoja na kutoa maagizo hayo Rais Magufuli amewaondoa shaka watanzania juu ya upungufu wa sukari, kuwa serikali imeagiza sukari kutoka nje ya nchi ambayo itasambazwa kwa wananchi kwa bei nafuu ili kufidia upungufu uliopo.

"Wale wote waliokuwa wameficha sukari waiachie, wasipoiachia sukari, huwezi kuificha kama sindano, nimeshaagiza vyombo vya dola, vikague magodown yote, atakayekutwa na sukari ameificha, yule ni mhujumu uchumi kama wahujumu wengine, asije akanilaumu, asijee-akanilaumu, na ninasema kwa dhati, wewe mfanyabiashara uliyepata nafasi ya Tanzania kuleta bidha za sukari, halafu unanunua unakwenda kuficha ili kusudi wazee hawa wahangaike, ili mwezi mtukufu wa Ramadhani utakapoingia watu wakose sukari, dawa yao ninayo" Amesema Rais Magufuli.

Aidha Rais amewataka watanzania kuendelea kumuunga mkono na serikali yake na kumwombea kwa kufanya hivyo hatawaangusha.