Friday , 22nd Feb , 2019

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, George Kyando amethibitisha kutokea vifo vya watu 19, baada ya kutokea kwa ajali ya iliyohusisha gari aina ya Lori namba T 825 CMJ iliyoligonga gari lenye nambari T 269 CJC aina ya Coaster.

Akizungumza na www.eatv.tv Kamanda Kyando ameeleza ajali hiyo imetokea usiku wakuamkia leo majira ya saa 3 usiku katika eneo lenye mwinuko mkali katikati ya mpaka wa Mbeya na Mkoa wa Songwe ambapo mpaka sasa jeshi hilo linaendelea kuhakikisha barabara ya sehemu ajali ilipotokea inaweza kupitika.

"Ajali ilitokea mnamo majira ya saa 3.15 jana usiku baada ya gari aina ya lori kufeli breki na kuligonga kwa nyuma gari la aina ya Coaster lililokuwa na abiria 17 ambao wote walifariki papohapo", amesema Kamanda Kyando.

"Kati yao abiria wengine wawili akiwemo dereva wamefariki wakiwa hospitali, lakini natoa wito kwa madereva wafuate sheria za barabarani hasa wanapofika maeneo yenye mwinuko mkubwa, na niwaombe ndugu wajitokeze kuitambua miili ya ndugu zao", ameongeza Kamanda Kyando.

Kwa sasa miili ya watu hao 17 imehifadhiwa Hospitali ya Wilaya ya Mbozi kwa ajili ya uchunguzi.

Wakati huohuo Rais John Magufuli ametuma salamu za rambirambi kwa watu wa karibu na zilizopoteza ndugu na jamaa zao katika ajali hiyo iliyotokea mpakani mwa Mkoa wa Songwe na Mbeya na kusababisha vifo vya watu vya watu 19.

Taarifa iliyotolewa leo Ijumaa Februari 22, 2019 na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa imeeleza Rais Magufuli amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Brigedia Jenerali mstaafu Nicodemas Mwangela kufikisha salamu zake za pole.

Aidha imeeleza kuwa Rais Magufuli amezitaka mamlaka zinazohusika na usalama wa barabarani mkoani Songwe kufanya uchunguzi wa ajali hiyo na kuchukua hatua zinazostahili.