
Akizungumza na waandishi wa habari kijijini kwake Namahema ‘A’ wilayani Ruangwa mkoani Lindi leo jioni, Waziri Mkuu amesema fomu hizo zilipokelewa jana na amekwishapatiwa barua ya kupokea tamko hilo.
“Nimetekeleza takwa hilo la kisheria na tayari Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma imekiri kupokea tamko langu kwa barua iliyoniandikia kunijulisha kuwa imepokea tamko langu,” amesema Waziri Mkuu.
“Kwa kuzingatia mfano ulioonyesha na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli, ninawaagiza viongozi wote wanaotakiwa kujaza fomu hizo kwa mujibu wa sheria wafanye hivyo na kuziwasilisha ifikapo tarehe 31 Desemba, 2017 saa 10 jioni,” amesisitiza Waziri Mkuu.
Amewataja viongozi hao kuwa ni Mawaziri, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu, Naibu Makatibu Wakuu wote na viongozi wote walioko kwenye ngazi za uteuzi na kuwataka wahakikishe wanatimiza takwa ambalo lipo kwa mujibu wa kifungu cha 9 na cha 11 cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Na. 13 ya Mwaka 1995.