
Hayo yamesemwa leo Jijini Dar es Salaam na Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philipo Mpango wakati akitoa mwenendo wa hali ya uchumi na utekelezaji wa bajeti ya Serikali kwa mwaka 2017/2018.
Dkt. Mpango amesema katika tathimini iliyofanyika mwezi Novemba mwaka huu inaonesha kuwa uwiano wa deni hilo na pato la Taifa ni asilimia 32.5 likilinganishwa na ukomo wa asilimia 56.
“Katika kuangalia ukomo wa deni hili ambao uko chini, inaonesha kuwa deni hili ni himilivu katika kipindi cha muda wa kati na muda mrefu”, amesema Dkt. Mpango.
Aidha Waziri Mpango ameongeza kuwa Serikali tangu ifanikiwe kuziba mianya ya rushwa na ufisadi imefanikiwa kukusanya trilioni 1.2 kila mwezi. Pia amewapongeza walipakodi nchini na kuwataka Watanzania kujenga tabia ya kulipa kodi kwa maendeleo ya nchi.
"Naipongeza Benki Kuu ya Tanzania kwa usimamizi mzuri wa Sera za Fedha, kuanzia Disemba 12 mwaka huu BOT imeshusha riba inayoitoza Serikali katika mikopo kutoka asilimia 6.5 hadi asilimia 3 ili kuchochea utoaji wa mikopo katika uchumi," amesema Dkt. Mpango.