Thursday , 21st Jul , 2016

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu vijana,Ahmad Alhendawi amesema wakati umefika wa kuacha kurushiana lawama kuhusu chanzo cha ukosefu wa ajira kwa vijana duniani na badala yake hatua stahili zichukuliwe ili kuweza kufanikisha malengo.

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu vijana, Ahmad Alhendawi

Kwa siku tatu vijana kutoka pande mbali mbali za dunia wanakutana jijini Nairobi, kwenye jukwaa la kwanza kabisa la vijana kwenda sambamba na mkutano wa kamati ya biashara na maendeleo ya Umoja wa Mataifa, UNCTAD.

Ahmad Alhendawi, baada ya kuzungumza nao, ukosefu wa ajira ukiwa tatizo kubwa, amesema, kila mtu anarushia lawama mwenzake; waajiri wanadai vijana hanawa stadi, vijana wanasema hawapati mitaji, sekta binafsi inadai sera si rafiki..vijana wakisalia kuwekwa rehani kutokana na ukosefu wa uratibu wa mipango.

Mjumbe huyo amesema kuwa inapaswa kuwaleta hawa wadau pamoja na vyuo vya elimu, sekta binafsi na wadau wa biashara pamoja na serikali na wadau wa maendeleo ili wazungumze pamoja ili hatimaye sera wanazobuni ziwekeze zaidi kwa vijana.