Monday , 22nd Feb , 2016

Msanii Madee wa Tip Top amesema hajachukizwa na kitendo cha Dogo Janja kuitukana Tip Top na kusema kuwa ilikuwa ni mbinu ya kupata msichana aliyekuwa anamfukuzia, ingawa ni utovu wa nidhamu.

Madee ameyasema hayo alipokuwa akiongea kwenye kipindi cha Planet Bongo kinachorushwa na East Africa Radio, na kusema kuwa yeye binafsi hakijamkera na hana tatizo na Dogo Janja, lakini hajui kwa upande wa wenzake walioko kwenye kundi hilo la Tip Top Conection watakuwa wamelichukuliaje.

"Ni ukosefu tu wa nidhamu na sidhani kama ni ishu kubwa sana kwangu binafsi, sijui kwa wenzangu ambao wako TipTop wameibebaje lakini mi kwangu naona ni ishu flan ya kawaida, kwa sababu najua plan ambayo alijaribu kuongea dogo Janja ni katika angle nyingine, yani alikuwa anatafuta kitu ambacho alidhania yeye akiongea hivi ndo atafanikiwa kupata kile ambacho anakitaka kwa yule mdada, kwa hiyo mimi nachukulia kama alikuwa anamdanganya mwanamke", alisema Madee.

Pamoja na hayo Madee amesema kitendo hicho si ajabu kwa Dogo Janja kukifanya, kwani hata wao watu wazima hutumia mbinu zaidi ya hizo kumpata mwanamke, lakini milango ya kutoa ngoma ya Dogo Janja iko pale pale.

"Sawa kazitoa siri za Tip Top ndiyo, lakini hata sisi muda mwingine tunaongea vitu vikubwa zaidi hata ya vile ili kumhadaa mwanamke, kwa hiyo mi kwangu sichukulii kama ni ishu kubwa saana, na plan yake ipo vile vile tutarelease tu nyimbo yake soon tu", alisema Madee.

Wiki iliyopita Dogo Janja alisikika akitoa maneo akimwambia mwanamke na kusema kuwa sababu zinazopelekea yeye kutotoka kisanaa ni uongozi wake wa Tip Top kumbania, na kudai bora angebaki mwenyewe bila uongozi.