
Lupita Nyon'go akiwa na wazazi wake
Akizungumza Jijini Dar es Salaam, kwenye hafla maalum ya uzinduzi wa tamasha hilo la 17, kwa waandishi wa habari iliyofanyika kituo cha utamaduni cha Goethe Institute, mkurugenzi mkuu wa tamasha hilo, Profesa Martin Mhando, amesema Tamasha la Kimataifa la filamu la Zanzibar (ZIFF) la msimu wa mwaka huu litakalofanyika Kuanzia Juni 14 hadi 22, na linatarajiwa kuwa moto kwani linakuja na mambo mbalimbali yenye kuleta mabadiliko ya hali ya juu.
Tukio kubwa ambalo kwa sasa Tanzania hasa kwenye viunga vya Zanzibar na nchi nyingine duniani katika tamasha hilo la 17, ni ujio wa msanii mwenye asili ya Kenya na Mexico, mshindi wa tuzo ya Oscar na nyingine nyingi Lupita Nyong’o, anayetarajiwa kuhudhuria utoaji wa tuzo hizo za ZIFF mwaka huu, pamoja na wazazi wake Dorothy na Prof. Peter Anyang’ Nyong’o.
Mbali na Lupita, katika kuongeza utamu wa tamasha hilo, mastaa wengine nguli wa Afrika kwa mwaka huu wanaotarajiwa kuwapo katika ushuhudiaji wa utoaji wa tuzo hizo ni pamoja na muigizaji na mwanamitindo nyota wa Nigeria, Genevieve Nnaji.
Wengine ni Amr Waked (Misri), Faouzi Bensaidi (Morocco), Nadia Buari, Richard Mote Damijo ‘RMD’, John Dumelo, Desmond Eliot na Florence Masebe.