Friday , 19th Jan , 2018

Msanii wa Bongo Fleva anayechipukia Edu Boy amezua tafrani baada ya kuendelea na kazi ya 'ku-diss' wasanii wenzake wakiwemo wenye majina makubwa baada ya kufanya hivyo tena kwenye ngoma yake mpya 'Tunasafisha'.

Edu Boy amefunguka kwenye eNEWZ kwamba hajutii kuwadiss au kuwaimba wasanii wenzake kwenye nyimbo zake kwa kuwa kafanya hivyo ni kama msanii mwingine anavyoweza kuamua kuimba mapenzi na akaelezea ukweli kuhusu mapenzi na watu wakaelewa ujumbe wake.

Kwenye ngoma hiyo mpya aliyowashirikisha Belle 9 na Amber Lulu, Edu Boy amesikika akitaja majina kadhaa makubwa kwenye kiwanda cha mziki kama Ommy Dmpoz, Ney Wa Mitego, Joh Makini, Stamina, Young D, T Touch, Jux na wengine.

''Ila kitu ninachokiimba kwenye nyimbo zangu ni ukweli mtupu na kama kuna msanii anasema 'ameni-mind' aandae pambano ili ajulikane nani mbabe maana sitaacha kuimba mpaka zile tabia mbaya za watu maarufu kwenye jamii ziishe na kupotea kabisa kwa namna yeyote ile''. amefunguka mkali huyo kutoka Rock City.

Edu pia amewashukuru mashabiki zake kwa mapokezi mazuri ambayo ameyapata kupitia wimbo wake mpya 'Tunasafisha' huku pia akiwashukuru mashabiki wote ambao wamekuwa wakimpa ushauri na hata wengine wanao mtukana ila yeye anawachukulia poa tu.