Wednesday , 28th Feb , 2018

Klabu ya soka ya Yanga kupitia kwa msemaji wake Dismas ten amesema mshindi wa mchezo wao leo, ligi kuu soka Tanzania bara dhidi ya Ndanda FC atapatikana kutokana na maandalizi ya timu hizo.

Ten amesema hayo kwenye mahojiano na wanahabari kuelekea mchezo huo wa raundi ya 19 leo jioni ambapo Yanga itakuwa ugenini kwenye uwanja wa Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara.

''Ligi msimu huu ina ushindani mkubwa na haijalishi unacheza nyumbani au ugenini, maandalizi ya timu ndiyo yanaamua kama unashinda au utafungwa, na sisi tumejiandaa vyema kwajili ya kushindana na kupata ushindi'', amesema.

Yanga imetua Mtwara tangu juzi ikitokea mkoani Songea ambapo ilicheza na Majimaji FC kwenye mchezo wa kombe la shirikisho na kuibuka na ushindi wa mabao 2-1, ikifanikiwa kutinga hatua ya robo fainali.

Yanga ipo katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi ikiwa na alama 37, nyuma ya Simba SC yenye alama 45 kileleni huku ikiwa na michezo 19 idadi ya mechi ambayo Yanga inaifiksha leo.