
Kikosi cha Azam FC
Azam FC inaongoza mpaka sasa katika msimamo wa ligi kuu Tanzania bara kwa jumla ya alama 30 baada ya kucheza michezo 12 huku wakiweka rekodi nzuri ya kutopoteza mchezo wowote mpaka sasa.
Akizungumza Jijini Dar es salaam, Afisa habari wa Azam FC, Jaffari Idd Maganga amesema kuwa hakuna ubishi kwa sasa kikosi chao ni bora na endapo kutatokea matatizo ya kiasili nchini, basi watakuwa mabingwa kwakuwa wanaoongoza ligi mpaka wakati huu.
"Kwa sasa ipo wazi sisi ndio mabingwa maana kama bahati mbaya kutatokea na majanga ya asili, basi bingwa ni Azam FC, nasi tutawaakilisha nchi kwenye michuano mikubwa tunapaswa tuheshimiwe," amesema.
Azam FC inatarajia kushuka dimbani kesho, Alhamisi dhidi ya Ruvu Shooting, mchezo utakaopigwa katika uwanja wa Chamazi majira ya saa moja usiku ikiwa ni mwendelezo wa ligi kuu baada ya mapumziko kupisha michezo ya kimataifa.