
Mmoja wa wachezaji wa Bball Kitaa akionyesha umahiri wake katika kuruka na kufunga mtindo wa Slum Dunk.
Waandaaji wa mashindano mbalimbali ya mpira wa kikapu maarufu cha mtaani maarufu kama Bball kitaa mwishoni mwa juma hili wamefanya mashindano maalum ya kuashiria ufunguzi wa ligi ama mashindano ya Bball Kitaa yajulikanayo kama slum dunk ambayo hufanyika mara chache sana hapa nchini.
Mashindano hayo yalikuwa na washiriki kutoka timu tofauti tofauti akiwemo pia mshindi wa mwaka jana Baraka Mopele.
Ryan Rose mwenye umri wa miaka 19 tu mkazi wa mikocheni ndo akaibuka mshindi wa mashindano hayo na kujipatia kitita cha pesa taslimu ya kitanzania shilingi 500,000/= baada ya kuonyesha uwezo mkubwa sana katika kuruka mtindo huo wa Slum Dunk ambao ni maarufu sana nchini Marekani katika ligi ya mpira wa kikapu nchini humo NBA.
Akizungumzia shindano hilo Mratibu ama Muaandaji wa mashindano hayo Karabani Karabani amesema mashindano hayo ni kwa ajili tu ya kuendelea kuwapa burudani wapenzi wa mchezo huo kabla ya ligi ya yenyewe ya Bball Kitaa inayokuja mwezi wa saba mwishoni haijaanza rasmi.
Mashindano hayo pia yalihudhuriwa na baadhi ya viongozi wa Basketaball Tanzania akiwemo Rais wa Basketball Dar es Salaam-BD Mwenza Kabinda ambaye amewasihi watu wengine wengi zaidi kujitokeza na kuandaa mashindano mengi ya kikapu na wao watawaunga mkono ili kuinua mchezo huo hapa nchini.
