
Viswanathan Anand. Bingwa wa dunia mara tano.
Mwenyekiti wa chama cha mchezo wa Chess Tanzania TCA bwana Geofrey Crispin Mwanyika amesema ujio wa wachezaji wakubwa wa kimataifa wa mchezo huo unasaidia kuhamasisha kuutangaza na kuukuza mchezo huo hapa nchini. Bwana Mwanyika aliyasema hayo wakati akizungumzia ujio wa bingwa wa dunia mara tano wa mchezo huo kutoka India bwana Viswanathan Anand ambaye yupo nchini kuhamasisha mchezo huo.
Anand yupo nchini kwa ziara ya siku tano kwa mwaliko wa mwenyekiti wa mfuko wa maendeleo ya Chess nchini Tanzania Chess Foundation TFA bwana Vinay Choudhury ambaye pia ni mjumbe wa chama cha mchezo huo hapa nchini TCA.
Anand atashiriki mashindano yaliyopewa jina la Chess kwa maafisa watendaji yaani ma-CEO hapo kesho. Mashindano hayo ni maalumu kwa ajili ya kuchangisha fedha itakayosaidia kuinua mchezo huo.
Kesho hiyo hiyo pia kutakuwa na mashindano ya Fide Rating kati ya Tanzania na Kenya ambayo ni maalumu kwa ajili ya kuwatafutia viwango wachezaji wa Tanzania ili watambulike na shirikisho la dunia la mchezo huo, FIDE. Tanzania haina hata mchezaji mmoja mwenye kiwango cha kutambuliwa na shirikisho hilo