Sunday , 7th Jan , 2018

Baada ya klabu za Barcelona na Liverpool kufikia makubaliano ya nyota wa Brazil Philippe Coutinho kutua Camp Nou, kiungo huyo anakuwa nyota wa pili kununuliwa kwa fedha nyingi zaidi katika historia ya soka.

Nyota huyo amekamilisha vipimo vya afya jijini Barcelona usiku wa kuamkia leo na atasaini mkataba wa miaka mitano na nusu. Coutinho ameigharimu Barcelona kiasi cha £142m, takribani shilingi milioni 383.

Barcelona itaanza kulipa kiasi cha £ 105m na kiasi kingine kitakuwa kinalipwa kutokana na kiwango atakachoonesha nyota huyo mwenye umri wa miaka 25. Coutinho alisajiliwa na Liverpool Januari 2013 kutoka Inter Milan kwa dau la £ 8.5m.

Coutinho sasa anakuwa mchezaji wa kwanza kutoka ligi kuu ya England kuuzwa kwa fedha nyingi rekodi ambayo ilikuwa inashikiliwa na Gareth Bale ambaye alinunuliwa kwa dau la £80m kutoka Tottenham kwenda Madrid.

Coutinho pia anakuwa mchezaji wa pili kusajiliwa kwa gharama kubwa akitanguliwa na Mbrazil mwenzake Neymar ambaye alisajiliwa na PSG kutoka Barcelona kwa dau la £222m.

Philippe Coutinho anaweza kuzidiwa na nyota wa PSG Kylian Mbappe ambaye amenunuliwa kwa mkopo kutoka Monaco lakini atanunuliwa kwa dau la £166m msimu ujao.