Friday , 22nd Dec , 2017

Klabu ya soka ya Singida United imeendelea kuonesha jeuri kwa vilabu vikubwa vya Tanzania na Afrika baada ya kufanya usajili wa beki Malik Antri kutoka Ghana.

Singida kupitia taarifa yake iliyoitoa leo imeeleza kuwa imefanikiwa kupata saini ya mlinzi huyo wa kati ambaye anacheza katika kikosi cha timu ya taifa ya Ghana ya wachezaji wa ndani (CHAN).

“Tunapenda kuwafahamisha kuwa tumekamilisha usajili wa beki wa kati wa timu ya Taifa ya Ghana (CHAN) Ndg. Malik Antri ambaye hii leo amewasili Singida”, imeeleza taarifa hiyo.

Aidha Singida United inayofanya vizuri msimu huu ikiwa katika nafasi ya nne hadi sasa imeachana na mlinzi wake Elisha Muroiwa ambaye amerejea kwao Zimbabwe kwa matatizo ya kifamilia hivyo nafasi yake kuchukuliwa na Malik Antri.

Klabu hiyo inayowakilisha kanda ya kati leo itashuka dimbani kukipiga na klabu ya Bodaboda FC kwenye mchezo wa kombe la shirikisho. Mchezo huo utapigwa kwenye dimba la Namfua mjini Singida.