Tuesday , 23rd Jan , 2018

Shirikisho la Mpira wa Miguu Barani Africa (CAF)limemteua Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania TFF Ahmed Mgoyi kuwa Kamishna wa mchezo wa Kombe la Shirikisho.

Mgoyi atakuwa Kamishina wa mchezo namba 13 kati ya AFC Leopards ya Kenya na Fosa Juniors ya Madagascar.
Mechi hiyo itachezwa kati ya Februari 9,10 na 11 mwaka huu nchini Kenya. Kwenye mchezo huo waamuzi wote wanatoka nchini Somalia ambapo mwamuzi wa kati ni Abdulkadir Artan Omar.

Mgoyi ni miongoni mwa Wajumbe wa Kamati ya utendaji wa TFF walioteuliwa hivi karibuni kuwa makamishna wa mechi zinazoandaliwa na CAF kwa mwaka 2018 mpaka mwaka 2020, wengine ni Makamu wa Rais wa TFF Michael Wambura, Amina Karuma na Sarah Tchao.

Wakati huo  Rais wa TFF  Wallace Karia yupo nchini Morocco ambako ameteuliwa kwenye kamati ya mashindano ya fainali za Africa kwa wachezaji wanaocheza ndani CHAN zinazoendelea nchini humo.

Tayari Karia ameshasimamia mechi mbili za CHAN ikiwemo ya ufunguzi iliyowakutanisha wenyeji Morocco na Mauritania Januari 13 na mchezo wa pili uliochezwa jana Januari 22 kati ya Namibia na Zambia.