
Masoud amesema baada ya kujiunga na Simba alimkuta Gyan na baada ya kumtazama kwenye mazoezi alimtamkia kuwa hawezi kucheza soka wala hafananii kuwa mchezaji lakini kwasasa Gyan amemjibu kwa vitendo.
"Nilimwita Gyan na kuzungumza naye na nikamwambia wewe si mchezaji, inakuwaje haupigi pasi, wala hautulizi mpira vizuri, kwa sababu haiwezekani mchezaji awe anakosa vitu hivyo, lakini kumbe mwenyewe kichwani alikuwa anafikiria kuwa anarogwa," ameeleza Masoud.
Kocha huyo raia wa Burundi ameongeza kuwa baada ya kugundua kuwa Gyan anawaza hivyo alikaa naye na kumshauri kisha akampa nafasi ya kucheza na mwisho wa siku ameonesha kiwango kikubwa na amekuwa msaada kwa timu.
Masoud amekuwa akimtumia Gyan upande wa kulia kutokana na kasi yake ili kusaidia mfumo wake wa 4-4-2 ambao huwa unabadilika na kuwa 3-5-2 timu ikiwa inacheza hivyo Gyan mara nyingi husaidia kurudi kama mlinzi wa kulia na baadae kupanda kama winga.