
Kocha wa Azam akiongoza vijana wake katika mazoezi nchini Afrika Kusini
Mchezo huo wa raundi ya kwanza ya michuano hiyo, unafanyika katika Uwanja wa Taifa wa Somhlolo, mjini Mbabane, Swaziland utakaoanza saa 10.30 jioni kwa saa za Afrika Mashariki.
Azam FC kuelekea mchezo huo, ilikuwa imepiga kambi jijini Pretoria, Afrika Kusini tangu Jumatano iliyopita na imewasili nchini Swaziland jana Jumamosi wakiwa na morali kubwa ya kupata matokeo mazuri.
“Unapocheza ugenini unatakiwa kubadilisha baadhi ya vitu kwenye mbinu, nitafanya kazi na wachezaji kuhusiana na hilo wachezaji wamekuwa wakinisikiliza, nimeona wanavyonisikiliza, nawaamini wachezaji wangu, namuamini Mungu wangu nitapata matokeo mazuri na klabu ya Azam itashinda mchezo na kufuzu kwenye hii michuano". Amesema Cioba
Baada ya kuondoka na ushindi wa bao 1-0 kwenye mchezo wa awali, Azam FC inahitaji kupata ushindi wowote au sare yoyote ili kuweza kusonga mbele kwa hatua ya mwisho ya mtoano (play off).
Moja ya silaha kubwa za Azam FC katika kuhakikisha inasonga mbele ni kuhakikisha inapata bao la ugenini, ambalo litazidi kuongeza mlima kwa wenyeji hao kuweza kupenya kwa raundi ijayo.