Monday , 5th Sep , 2016

Wakufunzi wawawake wa kozi mbalimbali za ukocha wa mpira wa miguu hapa nchini wametakiwa kutumia elimu wanayoipata kuhamasisha na kuelimisha ili kuweza kuwa na makocha wengi wanawake hapa nchini.

Baadhi ya washiriki wa kozi ya ukocha pamoja na wakufunzi

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kozi ya makocha 26 wanawake iliyoanza hii leo jijini Dar es Salaamm Mjumbe wa Baraza la michezo nchini Jenipher Mmasi amesema, wanawake wanatakiwa kufanya kazi hususani za kufundisha soka bila kuangalia jinsia au anafanya kazi na nani ili kuweza kukuza na kuzalisha vipaji ambavyo hapo baadaye vitaleta faida kwa ajamii.

Jenipher amesema, wakufunzi wengi wamekuwa na tabia ya kukaa na vyeti ndani bila kufanya kazi waliyotumwa ili kuzalisha jamii ya soka hivyo kuchangia kushindwa kupata vijana wengi ambao wataendelea kutangaza nchi katika ramani ya soka.

Kwa upande wake mmoja wa washiriki wa kozi hiyo Mwajuma Noti amesema, anaamini mara baada ya kumaliza kozi hiyo watajitahidi kuhamasisha wanawake wazidi kujitokeza ili kuweza kuinua soka la wanawake hapa nchini.

Mwajuma amesema, anaamini kozi zitakavyozidi kutolewa kwa wingi kwa upande wa wanawake, wataweza kupata makocha wengi wanawake na hata vipaji vipya vingi hapa nchini.

Kozi hiyo ya siku nne ya Shirikisho la Soka Ulimwenguni FIFA, inatarajiwa kumalizika Septemba 09 mwaka huu.