Tuesday , 24th Jan , 2017

Shirikisho la Soka Tanzania TFF limetangaza maamuzi kuhusu mechi namba 38 ya ligi daraja la kwanza kati ya Lipuli na Mshikamano FC iliyomalizika kwa vurugu katika uwanja wa Kichangani mkoani Iringa, ikiwa ni pamoja na kumfungia mwamuzi wa mchezo huo.

Boniface Wambura - Mtendaji Mkuu Bodi ya Ligi

Taarifa ya TFF imesema kuwa mwamuzi Bryson A. Msuya amefungiwa mwaka mmoja kwa kutozingatia sheria ipasavyo wakati akitoa penalti dhidi ya timu ya Mshikamano FC, na ripoti yake kufanana na ile ya Kamishna.

Kocha wa Mshikamano FC Hamisi Kinonda amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 300,000 baada ya kuondolewa kwenye benchi kwa kupinga muda wa nyongeza wa dakika tano, na kumtolea lugha ya matusi Mwamuzi wa Akiba

Wachezaji wa Mshikamano FC, John Mbise jezi namba 9, Abdallah Makuburi (5), Ally Mangosongo (12) na kipa Steven Peter (1) wanapelekwa Kamati ya Nidhamu ya TFF kwa kumshambulia Mwamuzi Bryson A. Msuya.

Mwamuzi Msaidizi Namba Moja, Makongo Katuma amefutwa katika orodha ya waamuzi wanaotambuliwa na TFF kwa kuwapiga vichwa wachezaji wawili wa Mshikamano FC wakati Mwamuzi wa Kati alipokuwa akishambuliwa na wachezaji wa timu hiyo wakati wakipinga adhabu ya penalti dhidi yao.

Naye Mwamuzi wa Akiba, Hashim Mgimba ameondolewa kwenye ratiba kwa kuonyesha muda wa nyongeza (added time) tofauti na ule alioelekezwa na Mwamuzi. Adhabu dhidi ya Mgimba imezingatia Kanuni ya 38(1d) ya Ligi Daraja la Kwanza.

Kamishna wa mechi hiyo Fidelis Ndenga wa Njombe ameondolewa kwenye ratiba ya makamishna kwa taarifa yake kufanana na ile ya Mwamuzi. Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 39(1) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Udhibiti wa Makamishna.

Pia Kamati imetoa mwito kwa vyombo vya usalama (askari polisi) kutumia nguvu za wastani katika kutuliza ghasia viwanjani, hasa pale wanapotaka kushughulikia eneo linalohusu wachezaji.

Uwanja wa Kichangani umeondolewa kutumika kwa mechi za Ligi, hivyo klabu za Iringa sasa timu zao zitatumia Uwanja wa Kumbukumbu ya Samora mjini humo kwa mechi zao la Ligi. Uwanja huo ulikuwa kwenye matengenezo ambayo tayari yamekamilika.