Thursday , 20th Oct , 2016

Ratiba ya Ligi ya Soka la Wanawake Tanzania Bara inayotarajiwa kuanza kutimua vumbi Novemba Mosi mwaka huu imetajwa hii leo ambapo ligi hiyo itachezwa ikiwa katika makundi mawili.

Soka la wanawake

Afisa Habari wa Shirikisho la Soka nchini TFF Alfredy Lucas amesema, ligi hiyo itaanza ikiwa katika mfumo wa makundi A na B ambapo kwa upande wa viwanja pia kila kundi lina viwanja ambavyo vitatumika katika Ligi hiyo.

Kwa upande mwingine Lucas amesema, vipo vilabu vya Ligi hiyo ambavyo vilituma pingamizi kuhusu usajili wa wachezaji lakini vimeshindwa kutokana na kukosa vigezo huku klabu moja pekee ambayo ni Mburahati Queens ikiwa imekidhi vigezo vya wachezaji wake watano ndio watakaojadiliwa katika kikao cha kamati ya soka la wanawake kitakachofanyika Oktoba 22 mwaka huu.

Kundi A litakuwa na timu za  Viva Queens ya Mtwara, Mburahati Queens ya jijini Dar es salaam, Fair Play ya Tanga, Ever Greens ya Dar es salaam, Mlandizi Queens ya Pwani na JKT Queens ya Dar es Salaam ambazo zitatumia viwanja vya Nagwanda Sijaona jijini Mtwara, Mkwakwani jijini Tanga, Karume jijini Dar es salaam, Karume na Uwanja wa Uhuru vyote vya jijini Dar es Salaam.

Kundi B litakuwa na timu za Marsh Academy ya jijini Mwanza, Baobab ya Mjini Dodoma, Majengo Women ya Singida, Sisters ya Kigoma, Kagera Queens ya Kagera pamoja na  Panama FC ambapo kundi hili litatumia Viwanja vya CCM Kirumba Jijini Mwanza, Tanganyika mjini Kigoma na Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma.