Saturday , 3rd Mar , 2018

Afisa Habari wa Klabu ya Simba, Haji Manara amefunguka na kudai kutokuonekana uwanjani kwa Emmanuel Okwi na John Bocco ulikuwa ni mpango madhubuti wa benchi la ufundi ili kuwalinda wasiumie zaidi na kupelekea wakashindwa kucheza mchezo unaofuata.

Manara ametoa kauli hiyo leo (Machi 03, 2018) wakati alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari makoa makuu ya klabu hiyo eneo la Kariakoo Jijini Dar es Salaam na kuhusiana na mtanange wao dhidi ya Al Masry kutoka nchini Misri ambayo inatarajiwa kuingia nchini kesho (Jumapili) majira ya saa 12 jioni.

"Jana tulikuwa na majeruhi nasio kwamba majeruhi hawawezi kucheza asilimia 100 lakini technical la benchi yetu ikaona kutokana na hali ya Emmanuel Okwi na John Bocco wakaona ni heri wapumzike vizuri ili waje kucheza mechi kubwa lakini sio kwamba tuliidharau Stand United", amesema Manara.

Pamoja na hayo, Manara ameendelea kwa kusema "Jumatano Emmanuel Okwi, John Bocco watakuwa 'fit' kwa asilimia 100 ishallah, kwa hiyo watakuwepo uwanjani katika mechi hiyo. Haruna Ninyonzima amesharejea nchini kwa taarifa nilizo nazo na nimepewa ripota tena kuwa hakufanyiwa tena 'operation', amefanyiwa tu tiba ya kawaida ya hali ya juu na ameshaanza mazoezi tokea wakati yupo India".

Kwa upande mwingine, Manara amedai Haruna Niyonzima siku yeyote kutokea sasa anaweza kuungana na wachezaji wenzake kambini ili azidi kujiweka imara katika mchezo uliokuwa mbele wa Kombe la Shirikisho ambao unatarajiwa kuchezwa siku ya Jumatano (March 7,2018) katika uwanja wa Taifa Jijini Dar es salaam.