Tuesday , 6th Sep , 2016

Michuano ya Ligi kuu ya Soka Tanzania Bara inaendelea kesho Jumatano Septemba 7, kwa michezo mitatu kupigwa katika viwanja vitatu tofauti

Mechi ya Simba na Ruvu Shootimg, misimu miwili iliyopita

Michezo hiyo ni pamoja na Ruvu Shooting ambayo imeahidi kubeba pointi tatu mbele ya wenyeji Simba SC mchezo utakaopigwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es sa aalam.

Afisa Habari wa Ruvu Shooting Masau Bwire amesema wamejiandaa kwa ajili ya kushinda mchezo wa kesho na wataonesha ubora walionao kwa msimu huu kwa kubeba pointi tatu mbela ya Simba SC bila kujali kama wapinzani wao wamesajili wahezaji wakimataifa.

Masau amesema, tangu ligi imeanza hawajapoteza mechi kwa kufungwa hivyo katika mchezo wa kesho wanaamini maandalizi waliyoyafanya yatarudisha heshima ya timu hiyo mara baada ya dakika 90 za mchezo kukamilika.

Kwa upande wake Afisa Habari wa Simba SC Haji Manara amesema, mara baada ya kutoka sare katika mchezo uliopita dhidi ya JKT Ruvu kikosi kimejiandaa vizuri kwa ajili ya mchezo wa kesho na wanaamini matokeo yatapatikana baada ya dakika 90 za mchezo huo.

Manara amesema, wachezaji wote waliokuwa timu ya taifa wameshajiunga na timu na wanamalizia mazoezi ya mwisho jioni ya leo kwa ajili ya kuweza kupambana hapo kesho.

Michezo mingine ya ligi kuu inayotarajiwa kupigwa hapo kesho ni mabingwa watetezi Yanga wakiwa ugenini dhidi ya Ndanda FC Uwanja wa Nangwanda sijaona mjini Mtwara huku wajelajela Tanzania Prisons wakiwakaribisha Azam FC Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.