Saturday , 7th May , 2016

Kiungo Mcameroon wa Dinamo Bucharest, Patrick Ekeng amefariki hospitali baada ya kuanguka na kupoteza fahamu uwanjani wakati wa mchezo wa Ligi Kuu ya Romania jana.

Cristian Pandrea, Msemaji wa hospitali ya Floreasca, amesema Madaktari walijaribu kuokoa maisha ya kijana huyo wa umri wa miaka 26, lakini wakashindwa.

Dinamo ilikuwa inaongoza kwa mabao 3-2 dhidi ya Viitorul Constanta nyumbani wakati kiungo Ekeng anaanguka uwanjani dakika ya 69, zikiwa ni dakika saba tangu aingie kutokea benchi.

Ekeng alianguka katikati ya uwanja na mara moja wachezaji wa timu zote wakamzunguka.

Vyombo vya habari vya Romania vimeripoti kwamba alipata na tatizo la moyo na mara moja akakimbizwa hospitali, ambako umati wa mashabiki ulikuwa nje.

Patrick amewahi kuchezea klabu za Cordoba ya Hispania, Lausanne ya Uswisi, na Le Mans ya Ufaransa kabla ya kutua Dinamo mwaka 2016 ambako hadi anakutwa na umauti, alikuwa amecheza mechi saba.