
Rais Magufuli akikabidhi Sh milioni 50 kwa uongozi wa TFF
Kauli hiyo imetolewa na Rais wa TFF, Wallace Karia katika mahojiano na www.eatv.tv, ambapo amesema kuwa pesa hizo amekabidhiwa yeye na Rais Magufuli anaujua mpira tofauti na watanzania wengi ambao wanashabikia tu timu zao.
"Wanaozungumzia pesa alizotoa Rais waache kuzungumzia suala hilo kwa kuwa wanamsemea wakati yeye hajasema hivyo watulie, Rais anajua mpira na anafuatilia pia hivyo waache kufanya hivyo," amesema.
"Milioni 50 kazungumza, kanipa mimi na yeye kanyamaza mbona mnamsemea?. Rais anaujua mpira na anafuatilia mpira, na mimi nasema kwamba mhe. Rais ni mtu anayejua mpira kuliko hata watanzania wengi ambao wanajifanya wanajua mpira," ameongeza.
Pia Wallace Karia amesema kuwa wameumia kwa kupoteza mchezo wao dhidi ya Lesotho ila wanaamini kwamba Stars itafuzu michuano hiyo kwa kuweza kushinda nyumbani na kuwataka wanaozungumzia masuala ya pesa za Rais Magufuli waache kufanya hivyo.
Ikumbukwe Rais Magufuli alitoa shilingi milioni 50 kwa ajili ya maandalizi ya Stars kwa ajili ya mchezo wao dhidi ya Lesotho ambao Stars ilipoteza kwa kufungwa bao 1-0. Michezo ya mwisho ya hatua ya kufuzu michuano hiyo itachezwa mwezi Machi mwakani, ambapo Taifa Stars itacheza na Uganda katika uwanja wa taifa jijini Dar es salaam.