Simba na Kagera katika mchezo wa raundi ya kwanza
Simba itakuwa mgeni wa Kagera Sugar katika mchezo ambao unatarajiwa kuwa ni wenye ushindani wa hali ya juu hasa kutokana na uimara wa vikosi vya timu zote mbili hususani katika safu zao za ushambuliaji ambapo ile Kagera inaongozwa na Mbaraka Yusuph mwenye mabao 10 hadi sasa akiwa nyuma ya Shiza Kichuya wa Simba mwenye mabao 11.
Pia mechi hiyo inawakutanisha washambualiaji wawili ambao wametoka kupachika mabao katika mchezo wa Kimataifa wa kirafiki kati ya Taifa Stars na Burundi, ambao ni Laudit Mavugo (Simba) aliyeifungia Burundi na Mbaraka Yusuph (Kagera) aliyeifungia Taifa Stars.
Mechi hii pia inawakutanisha baadhi ya wachezaji wa Kagera Sugar ambao wamepitia Simba ambao ni golikipa Juma Kaseja, Ame Ally 'Zungu', Mbaraka Yusuph na Edward Christopher, huku kocha msaidizi wa Simba Mganda Jackson Mayanja akiwa anarejea katika timu aliyokuwa akiifundisha zamani.
Simba yenye point 55 inahitaji ushindi ili ifikishe point 58 na kurejea kileleni mbele ya Yanga ambayo baada ya ushindi wa jana, imefikisha point 56.
Mechi nyingine zinazopigwa leo ni African Lyon inayoikaribisha Stand United ya Shinyanga mchezo utakaofanyika dimba la Uhuru ambapo mchezo huu utaanza saa 8.00 mchana.
Mtibwa Sugar ya Morogoro watakuwa wageni wa Tanzania Prisons ya Mbeya kwenye Uwanja wa Sokoine jijini humo wakati Mwadui FC watawaalika JKT Ruvu ya Pwani kwenye Uwanja wa Mwadui huko Shinyanga huku Majimaji wakiwa ni wenyeji wa Toto Africans katika dimba la Majimaji mjini Songea.