Friday , 25th Aug , 2017

Rais wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), Gianni Infantino ametuma salamu za pongezi kwa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania, (TFF), Wallace Karia kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa (TFF) kwa kipindi cha miaka minne ijayo

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania, (TFF), Wallace Karia.

Katika salamu hizo, Rais Infantino amesema hana mashaka na uwezo wa Karia hasa ikizingatiwa alikuwa Makamu wa Rais wa Shirikisho hilo katika kipindi kilichopita hivyo anamini kuwa ataweza kuiletea nchi maendeleo kupitia mchezo wa soka.

"Kwa wakati wote nakuhakikishia ushirikiano wa kutosha kutoka FIFA katika malengo yako milango ya FIFA iko wazi,  wakati wowote waweza kuja kujadili masuala ya mchezo wa mpira wa miguu hasa eneo la utawala", alisema Rais Infantino.

Pamoja na hayo,  Rais Infantino ameweza kumualika Karia kuenda  kutembelea mji wa Zurich uliopo nchini Switzerland katika bara la Ulaya.

"Ningependa kuchukua nafasi hii kukualika kuja huku Zurich wakati wowote kuanzia sasa ambako nitapata  fursa ya kukutambulisha maeneo mbalimbali ya FIFA. Pia nimeagiza upande wangu wa utawala uwasiliane na wewe muweze kupanga tarehe rasmi ya safari. Nikutakie tena kheri na fanaka, nguvu na kila aina ya mafanikio katika majukumu yako mapya natarajia kuonana nawe kwa haraka", alisisitiza Rais Infantino.

Wakati huo huo, Shirikisho la Mpira wa Miguu la Rwanda (FERWAFA) nalo kwa upande wake limempongeza Rais wa TFF, Wallace Karia kwa kuchaguliwa kuwa kiongozi mpya wa shirikisho hilo.